UNICEF - Hata maji ya kutumia ndani ya familia yanageuka barafu kutokana na baridi kali Lebanon-

Share:

Listens: 0

Habari za UN

Miscellaneous


Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linaendelea kufanya kila jitihada kuwasaidia wakimbizi na raia wa Lebanon ambao wanakabiliana na  moja ya misimu yenye baridi kali zaidi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 10, huku theluji ikidondoka katika maeneo ambayo hayajashuhudia theluji kwa muongo mmoja. Taarifa zaidi anayo Anold Kayanda. Katika eneo la bonde la Bekaa, moja ya mikoa nchini Lebanon. Safu ya milima iliyogubikwa na baridi imelizunguka eneo hili lenye nyumba za maturubai nazo zikiwa zimezungukwa na theluji. Hali ni baridi mno na fauka ya hayo paa nyingine za nyumba zinavuja.  Familia za wakimbizi kutoka Syria pamoja na wenyeji wao ambao nao wamekuwa wakipambana na hali mbaya ya uchumi, sasa wanahangaika kujaribu kuiona kesho yao kwakuwa wanakumbana na baridi hili kali kuwahi kuonekana hapa katika miaka ya hivi karibuni.    Hali ya joto imeshuka mno kiasi cha kuwa chini ya nyuzi joto sifuri na kuacha wakimbizi wengi na familia za Walebanon zikihangaika kupambana na baridi. Wengine wanachoma moto karatasi na wengine kuni, ilimradi wapate joto kiasi. UNHCR inasema katika wiki iliyopita takribani familia 4,000 za wakimbizi ziliathiriwa vibaya na dhoruba hili la theluji na zinahitaji msaada.  UNHCR imeshuhudia, “hata maji ambayo watu wamejihifadhia majumbani kwa ajili ya matumizi yao, yameganda na kuwa vipande vya barafu.”   Shirika hili la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi na wadau wake wameendelea kutoa usaidizi wa mara kwa mara wa majira ya baridi pamoja na usaidizi wa dharura kama vile mahitaji kwa ajili ya malazi, blanketi za joto, vifaa vya usafi na kadhalika ili kusaidia familia katika wiki hii ngumu. Hata hivyo, inakuwa vigumu kuzifikia baadhi ya jamii kutokana na miundombinu ya mawasiliano kama simu na barabara kutatizwa na theluji kubwa.    Lebanon inakabiliwa na mzozo mkubwa wa kiuchumi ambao unaungana na idadi kubwa ya maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19. UNHCR imeingilia kati kutoa msaada angalau kwa wakimbizi na wenyeji wao na hadi sasa imewafikia watu 260,000 kuwapatia usaidizi katika majira haya ya baridi kali.